
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeendelea kuwavuta wasanii kujiunga na chama hicho, ambapo sasa wasanii wanne wa muziki wa kizazi kipya, maarufu Bongofleva na filamu, wanatarajiwa kutangazwa kuhamia chama hicho wiki hii.
Wasanii  hao wanadaiwa tayari kukubali kuingia kwenye chama hicho na  wanatarajiwa kutangazwa rasmi hadharani katika mkutano wa hadhara  utakaofanyika jijini Dar es Salaam.
Kukubali  kwao kuingia katika siasa, kunatajwa kutokana na ushawishi mkubwa  uliofanywa na wabunge vijana wa chama hicho, pamoja na Diwani wa CCM  kutoka kata moja ya Wilaya ya Kinondoni, ili chama hicho kivune kura za  vijana katika uchaguzi mkuu wa 2015.
Wabunge  hao wa Chadema na majimbo yao katika mabano ni Halima Mdee (Kawe);  Kabwe Zitto (Kigoma Kaskazini); John Mnyika (Ubungo) na Joseph Mbilinyi,  jina la kisanii Sugu (Mbeya Mjini).
Habari  kutoka kwa watu wa karibu na wasanii hao pamoja na ndani ya Chadema,  zinawataja wasanii hao kuwa ni wanamuziki Judith Wambura maarufu Lady  Jaydee na wa miondoko ya Hip hop, Selemani Msindi ama Afande Sele.
Taarifa  zinawataja wengine kuwa ni mwanamuziki Fredy Maliki maarufu Mkoloni na  mwigizaji wa filamu, Jacob Steven kwa jina la kisanii JB.
Inadaiwa  wasanii hao lengo la kuingia katika siasa kupitia chama hicho, ni  kuwania ubunge ambapo Jaydee anatajwa kutaka kugombea wilayani Musoma;  Afande Sele Morogoro Mjini; Mkoloni Jimbo la Tanga na JB Jimbo la Mkoa  wa Dar es Salaam.
Hata  hivyo gazeti hili lilipowatafuta kuzungumzia taarifa hizo wote walikana  ingawa wapo waliokiri kushawishiwa kuingia kwenye chama hicho na  viongozi wa Chadema na wananchi, ili wagombee ubunge.
 Afande  Sele alikana kujiunga na chama hicho na kusema hana taarifa hizo  isipokuwa ni kweli ameshawahi kufuatwa na viongozi wa Chadema wa Mkoa wa  Morogoro, wakimtaka ajiunge na chama hicho na agombee ubunge Morogoro  Mjini.
“Nimeshafuatwa  na viongozi wa Chadema wa mkoa na kata nijiunge na chama hicho na  nigombee ubunge …tena hata vijana wengi na baadhi ya wazee wamenitaka  nigombee ubunge kwa kupitia Chadema lakini nimekataa.
“Pia  Sugu ni mshikaji wangu na anapokuja Morogoro, vijiwe vyake ndio vyangu  naye vijana wameshamfuata wakimwambia anishawishi nigombee ubunge  kupitia Chadema, amekuwa akiniambia vijana wananitaka lakini mimi  sitaki, sijawahi kujiunga na chama chochote na naona mbunge wa sasa  (Abdulaziz Aboud) anafanya kazi nzuri.
“Mimi  sio mwanasiasa, lakini ni mwanaharakati kupitia muziki na mtandaoni na  nimekuwa nikitoa maoni mengi na kukosoa lakini narudia si mwanasiasa na  sijawahi kujiunga na chama chochote,” alisema Afande Sele.
Vilevile  amekanusha kushawishiwa na viongozi wa kitaifa wa Chadema au wabunge,  ingawa amekiri kuna wabunge wa chama hicho kuwa ni marafiki zake  wakiwemo Mbilinyi na Zitto.
Kwa  upande wa Jaydee alisema hafuati itikadi ya chama chochote cha siasa na  hapendi siasa kutokana na imani kuwa siasa ni uongo na yeye hapendi  uongo. Alisema hana nia ya kujiunga na chama chochote cha siasa wala  kugombea ubunge kupitia chama chochote.
Hata hivyo alipoulizwa iwapo atagombea baada ya Katiba kuruhusu mgombea binafsi, alisema kwa wakati huo atajua.
Hata  hivyo, Licha ya kuwaona wanasiasa ni waongo, anakiri wapo wanasiasa  anawaamini kutokana na kazi zao na kumtaja miongoni mwao ni Mwenyekiti  wa UDP, John Cheyo na Mbunge wa Afrika Mashariki, Shy-rose Bhanji.
Mwanamuziki  huyo alisema licha ya kuwa na marafiki wa Chadema na CCM kama Sugu na  Profesa Jay wa Chadema na Mbunge wa Viti Maalumu, Catherine Magige na  Bhanji wa CCM, hawajawahi kumshawishi kujiunga na vyama vyao. 
Mkoloni  Akizungumzia taarifa hizo za kujiunga na Chadema, JB alikana na kusema;  “mimi na siasa ni vitu tofauti, sijawahi kufuatwa na mtu wa Chadema na  angalau kungekuwa na dalili basi uniulize, hiyo ni taarifa ya  kutengenezwa na wewe ndiye uliyetengeneza hakuna aliyekupa ni udaku  huo.”
Kwa  upande wa Mkoloni, alisema hajawahi kufuatwa wala kushawishiwa kujiunga  na chama chochote, isipokuwa ni mwanachama wa muda mrefu wa Chadema na  amekuwa akishiriki kampeni, mikutano ya hadhara na matukio yote ya  uhamasishaji ndani ya chama hicho. 
Alisema  kuhusu kuombwa kuwania jimbo mkoani Tanga kwa tiketi ya chama hicho,  alisema hajawahi kuombwa na chama hicho kufanya hivyo.
“Sijawahi  kuombwa nigombee jimbo, na kuhusu nia ya kugombea, ni mapema mno  kuzungumzia suala hilo sasa na hata kanuni za chama changu haziruhusu  labda uniulize swali hilo mwakani naweza kuwa na jibu,” alisema Mkoloni.
Kwa  upande wake, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa, alikataa  kuzungumzia taarifa hizo akidai yuko barabarani na masuala yote  yanayohusu chama hicho aulizwe Msemaji wa chama hicho.
  
Hata  hivyo msemaji wa chama hicho, Tumaini Makene alisema hana taarifa  kuhusu kufanyika kwa mkutano wa chama hicho Dar es Salaam na kutaka  apewe muda afuatilie taarifa hizo.
-Habari leo
-Habari leo
 
No comments:
Post a Comment