KUNA jambo moja ambalo mashabiki wa timu ya soka ya Arsenal wa Bongo wanajivunia kwa sasa. Unajua hao mashabiki wamefanya nini? Wamegeuza kibwagizo cha wimbo maarufu wa ‘Personally’ unaotamba kwa sasa wakaupa jina la ‘Arsenally’.
Wimbo huo ni wa wakali wa muziki wa Afrika kwa sasa ambao ni Peter na Paul Okoye wa Nigeria. Kimuziki wakali hao wanajulikana kwa jina la P-Square.
Kwa sasa wamevunja rekodi ya kuwa wasanii ambao nyimbo zao hazijawahi kuachwa kupigwa kwenye majumba ya starehe tangu mwaka 2003 mpaka dakika hii unaposoma ukurasa huu.
Mwaka huo ndipo walipozindua albamu yao ya kwanza ‘Last Night’ ambayo ilitengenezwa na Timbuk Music Label.
Wasikilizaji wazuri wa muziki, watakumbuka kwamba tangu kutolewa kwa ngoma yao ya kwanza, kila mwaka wakali hao wanadondosha nyingine na mpaka sasa hawajawahi kupotea kwenye ramani.
Unaposoma makala haya, wimbo wao bora wa ‘Alingo’ unatesa na huku ‘Personally’ ukiendelea kupasua anga vilevile.
P-Square wametoka mbali mpaka kufikia hapo walipo sasa, kati ya mambo yaliyowawezesha kufikia mafanikio walionayo ni pamoja na kuwa na moyo wa kupenda kujifunza kutoka kwa wasanii wenzao waliowatangulia.
Walianza kuonyesha vipaji vyao tangu walipokuwa katika elimu ya sekondari nchini kwao Nigeria.
Waliwahi kujiunga na chama cha muziki na maigizo baada ya kupata mafunzo. Wakati huo waliimba na kucheza nyimbo za wasanii wa nje ya nchi yao kama vile Micheal Jackson, Bobby Brown na MC Hammer.
Mwaka 1997 waliunda kikundi kilichojulikana kwa jina la MMMPP, ikiwa ni majina yao na wenzao, M Clef a.k.a Itemoh, Micheal, Melvin, Peter na Paul. Kutokana na kumkubali sana Micheal Jackson, walianza kucheza Break Dance.
Mwaka 1999, P-Square walirudi katika shule ya muziki ili kujiendeleza katika mafunzo ya upigaji gitaa, kinanda, ngoma, filimbi na kadhalika. Mpaka sasa wao ndiyo wanamuziki nguli wanaomudu kupiga ala mbalimbali.
Baada ya hapo walijiendeleza na masomo katika Chuo Kikuu cha Abuja wakisomea masomo ya Utawala wa Biashara.
Ni hapo ndipo walipoanza rasmi kutumia jina la Double P&P, Da Pees na baadaye wakatulia na jina hili la P-Square chini ya udhamini wa Bayo Odusami ‘Howie T’ ambaye pia ni promota na CEO wa Adrot Nigeria Limited.
P-Square ya sasa ina albamu nne; ‘Last Night’, ‘Danger’, ‘Get Squared’ na ‘Game Over’.
Kwenye Get Squared ndiyo kuna ngoma kama Story, Bizzy Body, Get Squared, Say Your Love na Temptation. Kwenye Danger kuna nyimbo zilizowika pia kama vile I Love You, Possibility, Danger, No Easy na Gimme Dat.
Kwenye Game Over ndio walimaliza mchezo kiukweli. Humo kuna nyimbo kali kama vile No One Like You, Do Me waliyomshirikisha Waje, Ifunanya na Roll It.
Wamechukua tuzo zaidi ya 20 mpaka sasa huku wakiwa wasanii wanaomiliki studio yao wenyewe. Kwa jinsi walivyojitosheleza, kama unataka kuwachukua kwa ajili ya onesho unapaswa kutokuwa na chini ya Dola 300,000.
Kipya na kizuri ambacho kimeongezwa kwenye kundi la vijana hawa pacha ni jinsi maonesho yao yanavyokuwa, kuanzia mwezi Julai mwaka huu wamegoma kabisa kufanya muziki wa ‘Playback’.
P-Square wa sasa wanafanya onesho kwa saa tatu huku wakiwa na wanamuziki wenzao 11 na onesho lao halipungui saa tatu.
Ukizungumzia kipato, wanamuziki hawa tangu mwaka hu uanze, wamekuwa na onesho kubwa kila mwezi ambapo kwa wiki 52 za mwaka wanakisiwa wataingiza maelfu ya dola.
Pia wana ndege binafsi waliyonunua, jumba la kifahari walilolipa jina la Squareville, studio yao ya Square Records pamoja na mkataba mnono walionao na kampuni ya simu ya Globacom ya nchini Nigeria
No comments:
Post a Comment