Saturday, 21 September 2013

GHARAMA ZA MATIBABU MUHIMBILI ZAPANDA MARADUFU.....SASA KUMWONA DAKTARI NI SHILINGI 30,000/=


           Gharama za huduma  za kulipia matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili zimepanda maradufu.
Hatua hiyo inayotekelezwa bila kuwashirikisha wadau na watoa huduma ilianza Septemba mosi mwaka huu na kulalamikiwa na wagonjwa na wafanyakazi.

Kwa mujibu wa tangazo la Mkurugenzi wa MNH, lililobandikwa kwenye ubao wa matangazo wa jengo la mateniti la kulipia huduma  IPPM, inaonyesha kuwa gharama zilipanda kuanzia Septemba 2, wakati notisi hiyo iliyosainiwa na Mkurugenzi ilitolewa Septemba 4.

Wagonjwa wanaolipia matibabu  binafsi Muhimbili  waliliambia gazeti hili kuwa  wateja wanaotumia ‘ast truck’  na huduma ya uzazi inayotolewa na  kitengo cha mateniti- IPPM ndizo zilizoongezeka.
 
Kuanzia sasa upasuaji wazazi  unalipiwa Sh. 500,000 badala ya  350,000 za awali. Uzazi  wa kawaida  ni Sh. 250,000 badala ya  Sh. 150,000  zilizokuwa zikitozwa mwanzo.

Walisema kulala kunagharimu  Sh. 20,000  badala ya 15,000 wakati tozo la kumuona daktari kwa mara ya kwanza  ni Sh. 30,000 badala ya Sh. 20,000 za awali.  

Kumuona daktari kwa ajili ya kufuatilia huduma na matibabu zimepanda hadi Sh. 20,000 kutoka Sh. 10,000.

Huduma nyingine kama dawa na uchunguzi wa maabara 
zimepanda japo bei zake hazikutangazwa  kwenye ubao wa matangazo.

Kwa wagonjwa wa kujifungua kawaida ambao  hawalipii gharama  watatozwa gharama ambazo hazikafafanuliwa ingawaje serikali inataka watibiwe bure.

“Mfano mjamzito akipata uchungu ghafla na kufika Muhimbili bila rufaa atatakiwa kalipia gharama” alisema mjamzito jina tunalo.

Msemaji wa MNH Aminieli Aligaesha, alikiri kuongezeka gharama hizo ziliongezeka  na kuongeza kuwa sababu ya ongezeko  hilo ni gharama kubwa za uendeshaji.

Hata hivyo alikataa kutoa maelezo zaidi na kutaka mwandishi wetu kwenda ofisini kwake   kwa maelezo zaidi.

Hospitali ya Muhimbili inatoa huduma kwa utaratibu wa aina mbili kuchangia matibabu kunakofanywa na mgonjwa wa rufani pamoja na serikali.

Njia nyingine ni  wagonjwa kulipia gharama zote  za tiba kama ambavyo wanafanya kwenye hospitali za binafsi.

Hata hivyo gharama za tiba kwa wale wanaochangia matibabu na wale wa rufaa hazijaongezeka.

No comments:

Post a Comment