
JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limeleezea namna mwanajeshi wake, Meja Khatibu Shaaban Mshindo, alivyouawa baada ya kuangukiwa na bomu, wakati akiwa katika jukumu la ulinzi wa amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Pamoja  na hayo, Watanzania wametakiwa kuimarisha mshikamano na kuachana na  makundi yenye nia ya kuleta mgawanyiko, hasa katika kipindi hiki kigumu  ambacho Tanzania imepoteza askari wake waliopewa dhamana ya kitaifa ya  ulinzi wa amani katika nchi zenye migogoro Afrika.
Akitoa  salamu za rambirambi wakati askari huyo wa kikosi cha Mizinga namba 83  KJ kilichopo Kibaha akiagwa rasmi kijeshi Dar es Salaam jana, Mkuu wa  Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamnyange, alisema askari huyo pamoja  na askari watano wa Tanzania, waliangukiwa na bomu hilo na kujeruhiwa  vibaya.
“Waliangukiwa  na bomu Agosti 28, mwaka huu huko Goma DRC eneo walilokuwa wakifanyia  kazi… Meja Mshindo aliumia vibaya na kukutwa na mauti njiani akipelekwa  hospitalini,” alisema Jenerali Mwamunyange.
Alisema  katika tukio hilo, askari wengine watano wa Tanzania walijeruhiwa  vibaya na wanaendelea vizuri na matibabu nchini humo na hali zao  zinaendelea vizuri.
Akimzungumzia  Meja Mshindo, Jenerali Mwamunyange alisema katika uhai wake alikuwa  mchapakazi, muaminifu, hodari na mtiifu na kifo chake kimetokea wakati  jeshi linamhitaji.
“Kifo  chake kimeacha pengo ndani ya JWTZ na itachukua muda mrefu kuziba pengo  hili.” Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard  Membe, alisema kifo cha askari huyo ni msiba wa kitaifa na kumtaja Meja  Mshindo kuwa shujaa aliyekutwa na mauti wakati akitekeleza kazi  aliyotumwa na nchi yake.
Alisema  kifo hicho pamoja na vifo vya askari wengine saba wa JWTZ vilivyotokea  Darfur mwaka huu, ni chachu kwa Tanzania kuendeleza jitihada za kusaidia  nchi zenye migogoro na kuhamasisha amani Afrika.
“Serikali inapata matumaini namna Watanzania walivyosimama pamoja na kuunga mkono jeshi letu katika kipindi hiki kigumu. Ingekuwa nchi nyingine, haya yaliyotokea yangeleta mgawanyiko mkubwa miongoni mwa raia, lakini kwa hapa kwetu hali imekuwa tofauti,” alisema Membe.
Aliwataka  wachache wenye mawazo ya kutumia matukio hayo kuwagawa Watanzania,  waache mara moja nia yao hiyo, kwa kuwa moja ya kazi ambayo Tanzania  inayo, ni pamoja na nia yake ya kuhamasisha na kutangaza amani Afrika na  dunia kwa ujumla.
“Jamani  wajibu wetu ni kuhakikisha haya maeneo yenye migogoro yanakuwa na  amani, kule DRC hali ni mbaya, watu wanakufa kila kukicha na akinamama  na watoto wanabakwa na kudhalilishwa, sasa sisi kama taifa ni vyema  kujitokeza na kusaidia wenzetu,” alisisitiza.
Meja  mshindo, alizikwa jana nyumbani kwao Fujoni Zanzibar na ameacha mke  mmoja, Hawa Mnimbo na watoto watatu ambao ni Shaaban, Abuu na Samir  Mshindo.
 
No comments:
Post a Comment