Thursday, 22 August 2013

TUME YA KATIBA ISIKUBALI KUYUMBISHWA

Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Mzee Joseph Butiku amesema asingekubali kushiriki katika Tume hiyo kama angejua kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM), kingeingilia mchakato wa kupata Katiba Mpya unaoendelea nchini. Mzee Butiku alitoa kauli hiyo katika nyakati tofauti mkoani Tanga wakati alipokuwa akizungumza katika mikutano ya Mabaraza ya Katiba iliyofanyika mwishoni mwa wiki.

 
Alisema hakufurahishwa na kitendo cha CCM cha kutoa waraka kwa wanachama wake nchi nzima ili kuwashinikiza kutoa maoni katika Mabaraza ya Katiba kwa kufuata maelekezo ya viongozi wa chama hicho. Alisema angejua CCM ingefanya hivyo asingekula kiapo kufanya kazi hii katika Tume hiyo na kuvionya vyama vya CCM na Chadema kwamba Muungano hautaponywa na helikopta zinazoruka au vitabu vya waraka vinavyosambazwa.
Wengi tunamfahamu vizuri Mzee Butiku sio tu kwa uzalendo na ‘uumini’ wake katika Muungano, bali pia kwa kuwa mmoja wa viongozi wachache katika nchi yetu wanaoendelea kumuenzi kwa vitendo Baba wa Taifa, marehemu Mwalimu Julius Nyerere. Sauti yake ya kukemea wanasiasa wanaofanya vitendo vya kuvuruga mchakato wa Katiba na kuwadhalilisha wajumbe wa Tume hiyo kwa kuhoji uzalendo wao eti kwa kupendekeza muundo wa serikali tatu bila shaka inawakilisha sauti za wajumbe wote wa Tume hiyo.
Kama ambavyo tumekuwa tukisema kupitia safu hii, Tume hiyo inayoongozwa na Jaji Warioba na kusheheni wajumbe wenye rekodi za uzalendo, uadilifu na utumishi wa umma uliotukuka kama Dk Salim Ahmed Salim, Jaji Augustino Ramadhani na wengine wengi, imekusanya na kuratibu maoni ya wananchi kuhusu Katiba wanayoitaka. Kazi hiyo imefanyika kwa umakini mkubwa na uzalendo wa hali ya juu pasipo kupindisha maono na matazamio ya wananchi. Mapendekezo waliyoyatoa katika Rasimu ya Katiba Mpya kwa ujumla wake ndio msimamo wa wananchi.
Hivyo, kejeli za baadhi ya wanasiasa kwa Tume hiyo, kwa mfano, kwamba wanaotaka muundo wa serikali tatu ni ‘wazee wanaosubiri kufa’ au wanaotaka muundo huo ‘hawana akili timamu’ hakika ni kejeli zinazotoka kwa wanasiasa mufilisi wanaotaka kuwatisha na kuwakatisha tamaa wajumbe wa Tume hiyo ili walete mapendekezo yatakayotoa Katiba itakayoendelea kulinda masilahi yao. Kejeli hizo ni ishara ya kuweweseka kwa kutambua kwamba kwa mara ya kwanza nchi yetu itapata Katiba itakayoleta demokrasia ya kweli na usawa kwa wote.
Tumetiwa moyo na Tume hiyo ambayo imeendelea na msimamo wake kwamba itapendekeza Katiba itakayotokana na maoni ya wananchi badala ya maoni ya viongozi wa vyama vya siasa, asasi na makundi mbalimbali yasiyo na maoni wakilishi. Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Joseph Warioba juzi aliwashambulia wanasiasa na asasi mbalimbali wanaopinga Rasimu ya Katiba bila hoja za msingi na kueleza kuwa, Tume yake haitasikiliza kelele hizo kwa sababu hazina masilahi kwa wananchi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam juzi, Jaji Warioba alionya wanasiasa na wasomi kuacha kujadili Rasimu hiyo kwa mtazamo wa kiitikadi na mgawanyo wa madaraka kana kwamba Rasimu hiyo haina mambo mengine ya msingi. Sisi tunaipongeza Tume hiyo kwa kutanguliza masilahi ya wananchi badala ya watu wachache. Tunawaasa wajumbe wa Tume hiyo wasiingie katika mtego wa wanasiasa wa kuingia katika malumbano yasiyo na tija kwa wananchi.
Source:Mwananchi

No comments:

Post a Comment