Tuesday, 27 August 2013

MWANAMKE ALIYEPANGA KUMUUA MUMEWE AENDELEA KUSOTA RUMANDE.

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Arusha jana imekataa ombi la hati ya dharura ya dhamana ya mke wa mfanyabiashara maarufu wa madini mkoani Arusha, Janeth Jackson (32), anayedaiwa kupanga njama za kumuua mumewe wa ndoa.
Janeth na mshitakiwa wa pili, Novatus Elias kupitia Wakili wao, Samsoni Rumende waliwasilisha hati hiyo katika Mahakama Kuu, kuomba dhamana baada ya mahakama ya wilaya ya Arusha iliyoko Sekei, kuwanyima dhamana.
Mahakama iliwanyima dhamana washitakiwa hao, kwa maelezo kuwa kufanya hivyo ni kuharibu kesi, kwani kuna watuhumiwa wengine hawajakamatwa.
Hata hivyo, Jaji Mary Moshi alikataa kumjumuisha mshitakiwa wa pili katika hati hiyo, kwa maelezo kuwa wakili hakumjumuisha katika hati.
‘’Katika hati ya dharura, naona jina la mshitakiwa wa kwanza tu ndiye anayeombewa dhamana, lakini jina la mshitakiwa wa pili, Elias, haliko hivyo siwezi kusikiliza kwa kuwa ni kinyume na utaratibu,’’ alisema Jaji Moshi.
Pamoja na hayo, Jaji Moshi alimnyima dhamana Janeth kwa maelezo kuwa Wakili Rumende amefanya makosa ya kisheria, kwani alipaswa kukata rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama ya wilaya wa kumnyima dhamana mteja wake.
Alisema kuomba hati ya dharura ya kuomba dhamana, sio utaratibu wa kisheria na kutokana na hali hiyo, alimtaka wakili huyo kwenda kujipanga upya .
Awali akizungumza mahakamani hapo, Rumende alimwomba Jaji Moshi kumpa dhamana mteja wake, kwani ana mtoto mchanga wa miezi mitano.
Rumende alidai kuwa dhamana ni haki ya msingi ya mteja wake na hawezi kuathiri mwenendo wa kesi na atatii masharti ya dhamana kwa jamii, inayomzunguka bila ya wasiwasi wowote.
Hoja hizo zilipingwa vikali na Wakili wa Serikali, Edana Kasala aliyedai kuwa utaratibu umekiukwa na pili mahakama ya wilaya iko sahihi kuwanyima dhamana washitakiwa hao.
Janeth ambaye ni mkazi wa Moshono, jijini Arusha pamoja na Novatus Elias, katika kesi hiyo katika mahakama ya wilaya, wanashitakiwa kwa kula njama ya kutaka kumwua Jackson Manjuru ambaye ni mume wa Janeth.
Washitakiwa wote wawili pia wanadaiwa kutenda kosa la kula njama na kutaka kumwua Desderi Sabas, anayeishi Bukoba mkoani Kagera, ambaye ni mtoto wa nje wa mume huyo.
Washitakiwa wote hawakutakiwa kujibu lolote mahakamani hapo, kwa sababu Mahakama hiyo kisheria haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji.

Source: HABARI LEO

No comments:

Post a Comment