Saturday, 31 August 2013

HURUMA:MADAWA YA KULEVYA YANAWATESA WABONGO CHINA!

 
  
               Taifa la China halina mzaha mbele ya biashara haramu ya madawa ya kulevya na kwa kutambua kwamba wanaohusika zaidi ni Waafrika, sasa hivi kila mja mwenye ngozi nyeusi aliyepo nchini humo, anapewa msoto wa nguvu.
Wabongo wanaoishi China, kwa sasa wanahenyeshwa isivyo kawaida katika msako uliopewa jina
na Watanzania kwamba ni Oparesheni Safisha Wauza Unga.
Katika hoteli wanazofikia, vijiwe vyao, barabarani na kadhalika, kote huko wanapewa msoto wa guvu kwa kile kinachoelezwa kuwa Wachina hawana imani tena na Watanzania na Waafrika kwa jumla ama wanaoishi nchini humo au hata wale wanaoingia na kutoka.

“Wazungu wa unga (wafanyabiashara wa madawa ya kulevya) wanatuharibia starehe hapa China, hatuishi kwa amani tena. Mtu unaweza kukaguliwa siku nzima kisa eti wanawatafuta wanaouza unga,” alisema Artides Kimota ambaye ni Mtanzania anayeishi China kwa sasa.
Aliongeza: “Unajua sasa hivi China imekuwa na uingizwaji mkubwa wa madawa ya kulevya. Kwa Serikali ya China hii ni kashfa nzito. Kwa vile wanajua Waafrika ndiyo sababu kuu, sasa hivi kila Mwafrika anapewa msukosuko.

 
 “Kwa kweli ukiwa Mwafrika hapa China ni mateso makubwa sana kwa sasa. Kuna agizo la serikali ambalo limelitaka jeshi la polisi hapa China kuhakikisha madawa ya kulevya yanatokomezwa na wahusika wanakamatwa.

“Kila anayekamatwa na madawa ya kulevya au na kitu chochote ambacho siyo halali, anafunguliwa mashtaka. Mimi naishi kwenye Jiji la Qingyuan, nimeshahuhudia Mtanzania mmoja, Wanigeria wawili na Waghana watatu wakikamatwa.

“Kote hakuna kupumua, hata huko Guangzhou, Beijing na kwingineko kunatisha kwa msako. Nasikia kwenye Mji wa Shanwei alikamatwa Mtanzania mwingine, akakutwa na ungaunga wa marumaru ambao alikuwa nao kama sampuli kwa ajili ya biashara zake, alikamatwa lakini aliachiwa baada ya kupimwa na kugundulika siyo madawa ya kulevya.”
Habari zaidi zinasema kuwa pamoja na sifa mbaya ya Watanzania nchini humo lakini imebainishwa kwamba Wanigeria ndiyo kundi hatari na wanawindwa zaidi kwa sababu raia wa nchi hiyo wameshachafuka sana.
Imebainishwa zaidi kuwa kwa vile siyo rahisi kumtofautisha Mnigeria na Waafrika wengine kwa haraka, ndiyo maana kila Mwafrika anapoonekana ni lazima ale msoto wa kukaguliwa ili kuhakikisha kama ana ‘mzigo’ au hana.
Risasi Jumamosi linamiliki picha zinazowaonesha baadhi ya Waafrika wakiwa chini ya ulinzi, wakitembezwa vifua wazi, kueleka vituo vya polisi kufunguliwa mashtaka ya uhalifu mbalimbali ikiwemo madawa ya kulevya.

KINACHOWAPONZA NI HIKI
Kwa mujibu wa taarifa kutoka China, taifa hilo limeshtukia kwamba pamoja na sheria kali za udhibiti wa madawa ya kulevya zilizopo na adhabu kali ikiwemo ile ya juu kabisa ya kunyongwa hadi kufa kwa mtu anayekutwa na hatia ya kujihusisha na biashara hiyo, polisi wameendelea kupigwa bao la kisigino.
Imeelezwa kwamba watu wanaosafiri na madawa ya kulevya tumboni, maarufu kama punda ndiyo wanaofanya madawa yazagae nchini humo.
“Punda ndiyo wanatuponza, Serikali ya China imeshtukia kuona kwamba madawa yapo sana mitaani, kwa hiyo kukomesha kabisa hilo, wanafanya msako hatari sana. Wakifika chumbani kwako utajuta, wanapekua kila upande wa chumba.
“Vilevile ikitokea mtu anawasili uwanja wa ndege akiwa dhaifu, anafuatiliwa sana. Asikwambie mtu, hakuna Mwafrika aliyepo China anayeishi kwa raha, iwe unauza au huuzi lazima uhenyeshwe,” alisema Dominick Rafiki anayeishi Guangzhou, China.

CHINA YASISITIZA KUENDELEA KUNYONGA
Ripoti ya Shirika la Haki za Binadamu la Amnesty International mwaka 2012, iliitaja China kama taifa kinara kwa kunyonga watu wenye makosa mbalimbali na kuitaja nchi hiyo kama katili zaidi duniani.

Amnesty International inapingana na adhabu ya kifo, kwa hiyo imekuwa ikitumia jitihada mbalimbali kuhakikisha linaishawishi China iachane na hukumu za kunyonga watu bila mafanikio.
Shirika hilo lilieleza kwamba China imeendelea kuweka msisitizo wa kunyonga watu, huku ikiwa na rekodi ya kunyonga maelfu ya watu kila mwaka.
BALOZI AKIRI HALI NI MBAYA
Balozi mpya wa Tanzania nchini China, Luteni Jenerali Mstaafu, Abdulrahman Shimbo amekiri kwamba hali ni mbaya kutokana na wimbi kubwa la Watanzania kukumbwa na kashfa ya madawa ya kulevya, huku wengine wakiwa wameshahukumiwa kunyongwa.

“Ni kweli hali ni mbaya, kuna vijana wetu wengi wanaipa sifa mbaya nchi yetu hapa. Kama inavyofahamika, mimi bado mgeni lakini nikipewa muda kidogo nitakuwa na ripoti kamili ya jinsi Watanzania wanavyohusishwa na hii biashara haramu ya madawa ya kulevya,” alisema Balozi Shimbo ambaye alikuwa Mnadhimu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).
Source:GPL

No comments:

Post a Comment