Tuesday, 27 August 2013

SERIKALI YARUHUSU TENA MIHADHARA YA DINI ILIYOKUWA IMEPIGWA MARUFUKU.

MIHADHARA ya dini iliyokuwa imepigwa marufuku na Serikali imeruhusiwa kuendelea kwa masharti ya kutojihusisha na mahubiri yanayolenga kupandikiza chuki miongoni mwa Wakristo na Waislamu. Serikali pia imewataka viongozi wote wa dini kuwakataa na kuwapiga marufuku watu wanaojiingiza katika nyumba za ibada huku wakiwa na malengo ya siasa.

Akizungumza katika kongamano la Umoja wa Wahadhiri wa dini za Kikristo na Kiislamu Dar es Salaam juzi, Mkuu wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja alisema Serikali haiwezi kuingilia shughuli za dini kama zinaendeshwa kwa ustaarabu bila kuvunja sheria.

Chagonja ambaye alimwakilisha Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, Dk. Emanuel Nchimbi alisema Serikali haijawahi kupiga marufuku mihadhara yoyote inayoendeshwa bila kusababisha vitendo vya chuki na uhasama kwa Watanzania.

Kuruhusiwa kwa mihadhara hiyo kumekuja ikiwa imepita zaidi ya miezi minane tangu Serikali ilipopiga marufuku mihadhara hiyo nchi nzima ikiwa ni hatua ya kukabiliana na machafuko ya dini yaliyokuwa yanalinyemelea taifa.

Uamuzi huo ulichukuliwa siku chache baada ya baadhi ya waumini wa dini ya kiislamu kujiandaa kuandamana kwenda Ikulu kutaka atolewa rumande Kiongozi wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda.

Katika kongamano la juzi, Chagonja aliwaasa viongozi hao kuwa na mfumo mpya wa dhana ya uhalisia ya kutangaza dini na kuacha kukejeliana kati ya dini moja na nyingine kuepuka vitendo vya chuki za dini.

Kiongozi wa Mihadhara ya Kiislam, Naibu Amir, Shekh Rajabu Salum, alisema mihadhara ya pande zote mbili ijulikanayo kama ‘mihadhara linganishi’ haijawahi kuwa tishio la amani nchini.

Naye Mwenyekiti wa mihadhara ya Kikristo, Mwinjilisti Daniel Mwankemwa alisema mihadhara yao imetoa mchango mkubwa kwa waumini wao kuimarika kiroho baada ya kupata ufafanuzi sahihi wa hoja mbalimbali zilizokuwa zikiwasumbua.
Source:Mtanzania

No comments:

Post a Comment