Wednesday, 28 August 2013

CAG ADAI KWAMBA MAGUFULI SIYO FISADI.....ATOA UFAFANUZI WA KINA KUHUSU ZILE BIL. 252

MKAGUZI na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh amesema taarifa ya Sh bilioni 252 zilizokuwa zimeoneshwa katika taarifa ya Wizara ya Ujenzi, zilihamishwa kwenda Wakala wa Barabara (Tanroads) kulipia madeni ya wakandarasi na kwamba hapakuwa na ufisadi.
 

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Utouh alisema vyombo vya habari viliripoti suala hilo tofauti, baada ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) kukutana na wizara na kuhoji juu ya matumizi ya fedha hizo.
 
Utouh alisema baada ya PAC na Kamati ya Kudumu ya Serikali za Mitaa (LAAC) kupitia ripoti ya Wizara ya Ujenzi, kumejitokeza upotoshaji wa taarifa kuhusu hesabu za wizara hiyo na taarifa zisizo sahihi, zikidai kulikuwa na ufisadi.
 
Alisema fedha hizo zimeoneshwa kwenye taarifa ya hesabu za Wizara hiyo, kama vile ni miradi mipya ya mwaka 2011/2012 tofauti na uhalisia wake.
 
Utouh alisema uhalisia wa fedha hizo ni kuwa mara baada ya kupokewa na Wizara ya Ujenzi kutoka Hazina, zilihamishwa kwenda Tanroads kulipia madeni ya wakandarasi wa miradi ya barabara, iliyotekelezwa na wahandisi washauri, ambao walikuwa hawajalipwa kwenye mwaka wa fedha 2010/2011.
 
“Fedha hizi zilijumuishwa kimakosa kwenye hesabu za Wizara kama matumizi ya akaunti ya maendeleo, hivyo kuongeza matumizi ya Wizara kimakosa kwa kiasi hicho. 
Kihasibu fedha hizo zilipaswa kuoneshwa kwenye hesabu za mtumiaji halisi wa fedha ambaye ni Tanroads na siyo Wizara hiyo,” alisema Utouh.
 
Alisema kutokana na hali hiyo, hesabu za wizara hazikuwa sahihi, kutokana na uwepo wa ongezeko hilo kubwa la fedha na hivyo kusababisha kupewa hati ya ukaguzi yenye mashaka.
 
“Hivyo katika kujadili hesabu za Wizara ya Ujenzi hakukuwepo na tuhuma zozote za ufisadi, ila Kamati ya PAC ilimtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuihakikishia matumizi ya fedha hizo, jambo ambalo tumejiridhisha nalo kwa ushahidi wa namna mlolongo wake ulivyo hadi zilipotumika” aliongeza Utouh.
 
Aidha, alisema mbali na dosari hiyo ya kihasibu, Wizara ya Ujenzi inafanya kazi nzuri ya kusimamia na kujenga barabara katika kona zote za nchi, hivyo viongozi wake wanapaswa kupongezwa kwa kazi hiyo wanayoifanya huku akiwataka kuwa na moyo wa kuchapa kazi zaidi kwa ajili ya maendeleo ya taifa.
 
Katika hatua nyingine, Utouh alimpongeza Spika wa Bunge Anne Makinda kwa uamuzi wake wa kupanga upya Kamati za Kudumu ya Hesabu za Serikali Kuu (PAC), kwa madai kuwa utasaidia kuleta ufanisi na tija katika utendaji kazi wa kamati hiyo.
 
Alisema uamuzi wa Spika kuipanga upya PAC na kuwa na vyombo viwili PAC 1, itakayokuwa ikishughulikia taarifa za Hesabu za Serikali Kuu, idara zinazojitegemea na taasisi zingine za Serikali chini ya Mwenyekiti wake Zitto Kabwe na PAC 11, itakayokuwa ikishughulikia hesabu za Mashirika ya Umma chini ya uenyekiti wa Deo Filikunjombe, kutasaidia kuleta ufanisi mkubwa katika ufuatiliaji.
Source:Habarileo

No comments:

Post a Comment