Monday, 26 August 2013

NYUMBA 72 ZABOMOLEWA MKOANI MBEYA KUPISHA UJENZI WA BARABARA

NYUMBA 72 za makazi zilizopo eneo la Isanga jijini Mbeya, zimebomolewa kupisha upanuzi wa barabara yenye urefu wa kilomita zaidi ya 100, inayoanzia Mbeya kwenda Makongorosi, Wilaya ya Chunya. Bomoa bomoa hiyo ambayo ilianza jana majira ya saa mbili asubuhi na kusababisha vilio vya watu wa eneo la Isanga, ilifanyika chini ya usimamizi wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mkoa wa Mbeya. 
Akizungumza na MTANZANIA Jumatatu wakati wa bomoa bomoa hiyo, Mwenyekiti Msaidizi wa Kamati ya Waathirika wa tukio hilo, Ismail Mwaipaja, alisema Serikali kupitia TANROADS ilitoa taarifa ya kubomoa nyumba hizo mwaka 2010, baada ya kukamilisha taratibu mbalimbali za kisheria.

Alisema kwamba, Julai 28 mwaka huu, baadhi ya wahusika walipokea barua zikiwataka wahame katika makazi yao kwa kuwa bomoa bomoa ingefanyika mwezi huu.

Wakati wakiwa katika harakati za kutafuta haki zao kisheria, alisema walishangaa kusikia matangazo yakisema wanatakiwa kuondoka kwenye makazi hayo, kwani ubomoaji wa nyumba hizo ungefanyika jana.

“Tunachosikitika sisi ni zoezi hili kufanyika huku baadhi ya taratibu na vipengele vya kisheria vikikiukwa.

“Moja ya taratibu hizo ni ulipaji wa fidia kwa wamiliki wa nyumba, ambao umefanyika kwa baadhi ya watu na wengine bado hawajalipwa kwani kati ya nyumba 72 zilizothaminishwa kwa ajili ya kufidiwa, ni nyumba 29 tu ndizo zimefidiwa.

“Yaani hata zile zilizolipwa fidia, zimefidiwa kiwango kidogo kilichokuwa kinapingwa na wahusika.

“Pia, baada ya kuwapo kwa utata huu, wahusika tulijikusanya na kwenda kufungua kesi mahakamani na kesi inatarajiwa kusikilizwa kesho (leo), lakini tunashangaa kuona zoezi hili linafanyika wakati kesi iko mahakamani,” alisema Ismail.
 
MTANZANIA Jumatatu lilipotaka kujua undani wa tukio hilo kupitia kwa mmoja wa maofisa wa TANROADS aliyekuwa akisimamia bomoa bomoa hiyo, aliyejitambulisha kwa jina moja la Mhandisi Mkina, alikataa kuzungumzia suala hilo.

“Mimi si msemaji wa ofisi, subirini zoezi likamilike kisha mfike ofisini mkapate taarifa kamili,” alisema Mhandisi Mkina.
 
Naye Mwanasheria wa waathirika wa tukio hilo, Ladslaus Rweikata, alisema kitendo kilichofanywa na TANROADS kimekiuka sheria kwa kuwa suala hilo liko mahakamani.


No comments:

Post a Comment