Monday, 26 August 2013
NASIKITISHWA NA VITENDO VYA HUJMA Z’BAR-MAALIM SEIF
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema anasikitishwa na matukio ya hujuma yaliyojitokeza Zanzibar, ikiwemo watu kumwagiwa tindikali, na kutaka uchungunguzi wa kina ufanywe kuwabaini wahusika, na baadaye ripoti ya uchunguzi huo iwekwe wazi kwa wananchi.
Amesema hatua ya kuwekwa bayana ripoti za uchunguzi wa matukio hayo ya hujuma, ni jambo muafaka katika kufuta dhana zinazojengeka miongoni mwa wananchi na jamii ya kimataifa kuhusiana na watu wanaohusika kufanya hujuma hizo.
Maalim Seif ameyasema hayo katika mahojiano maalum juu ya maadhimisho ya miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar tangu kuasisiwa kwake mwaka 1964.
Amesema ili amani na mshikamano wa wazanzibari udumu, matukio kama hayo ya hujuma ambayo yamekuwa yakiwalenga zaidi baadhi ya viongozi wa dini na hata wageni, hayanabudi kuangaliwa kwa upana wake, na kuwataka wananchi wajiepushe na kufikia maamuzi ya haraka kuwahusisha wengine bila ya uchunguzi wa kina kufanywa.
Alisema wananchi walipata matumaini ya kukomeshwa kwa vitendo hivyo mara baada ya hujuma zilizofanywa dhidi ya viongozi wa dini pamoja na mripuko uliotokea katika kanisa la Arusha ambapo walihidiwa uchunguzi wa kina utafanyika na kuhusisha wapelelezi wa kimataifa, lakini hadi sasa hakuna ripoti yoyote iliyowekwa bayana.
Maalim Seif ameeleza kwamba badala yake matukio ya hujuma yameendelea na wananchi kuendelea kujenga dhana ya kuwahusisha watu au makundi maalum bila ya kuwa na uthibisho, jambo ambalo ni hatari kwa usalama na utulivu wan chi.
“Ingekuwa wakati ule tungesema ni siasa, lakini sasa tuna serikali ya pamoja Zanzibar, kwa nini mambo haya yanatokea sasa, huu ni mtihani mkubwa kwetu”, alisema Maalim Seif.
Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF, amesema pia amekuwa mgumu kuamini kuwa dini inahusika katika matukio ya hujuma yaliyotokea Zanzibar.
Amesema Zanzibar ina historia ya kipekee ya uvumilivu wa kidini duniani, kutokana na wananchi wa visiwa hivi kuishi pamoja kwa miaka mingi bila ya kubaguana kwa misingi ya dini zao.
“Sisi Zanzibar kiwango chetu cha uvumilivu ni kikubwa na nambari moja duniani, hata ukiangalia Ukristo Afrika Mashariki mlango wake ni Zanzibar”, alifafanua Maalim Seif.
Akitoa mfano wa uvumilivu huo, Maalim Seif amesema hata unafika mwezi wa Ramadhan huwezi kumuona mtu wa imani yoyote akila hadharani wakati wa mchana, na kwamba wananchi wote wanashirikiana katika shughuli za kijamii bila ya kujali imani zao.
Ameeleza kuwa baada ya matukio ya kujeruhiwa Padri Ambrose Mkenda, kuuawa kwa Padri Evarist Mushina mripuko wa bomu katika kanisa mjini Arusha, Serikali iliahidi kuleta makachero wa F.B.I, na hata baada ya wasichana wa Kiingereza kumwagiwa tindikali inaelezwa wachunguzi kutoka Scktland Yard wapo, lakini hakuna taarifa hadi sasa iliyotolewa kuhusiana na uchunguzi huo.
“Tusiajiegemeze kwenye dhana, uchunguzi ndio kitu muhimu. Hawa wanaoathirika na hujuma mbali ya kuwa viongozi wa dini nao ni binadamu, tujiulize jee hawakujenga uhasama au kutokufahamiana na wengine huko katika jamii”, alihoji Maalim Seif.
Amefahamisha kuwa ni makosa kuendesha mambo kwa dhana, kwa vile matokeo yake ni kuwaadhibu watu kwa kuwaweka ndani bila ya kuwa na hatia.
Amewataka wananchi kuwa makini na waendelee kuwa wamoja, ili amani, mashirikiano na umoja uliodumu uendelee wakati huu ambapo Zanzibar inaadhimisha miaka 50 ya Mapinduzi. Wakati huo huo Maalim Seif amekutana na Balozi mdogo wa China aliyepo Zanzibar Chen QiMan na kuelezea umakini na uadilifu wa makampuni ya Kichina katika kutekeleza majukumu yao.
Amesema mara nyingi kazi za kiufundi wanazopewa wataalamu wa Kichina zimekuwa zikitekelezwa kwa umakini na kwa wakati uliopangwa, hali inayotoa matumaini ya kuendelea kutoa tenda kwa makampuni hayo.
Aidha amesifu ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya China na Zanzibar ambao umekua ukichangia maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa jamii.
Amemtaka balozi huyo kuwa kiungo katika kuwashajiisha watalii na wawekezaji wa China kuja Zanzibar, ili kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali za kuwaletea wananchi maendeleo.
Amesema China ni mshirika wa kweli wa maendeleo ambayo imekuwa ikishirikiana na Zanzibar katika kutatua kero zinazoikabili ikiwa ni pamoja na kusaidia wataalamu hasa katika sekta ya afya.
Naye balozi QiMan amesema katika kipindi chake cha utumishi hapa nchini, ameshuhudia mafanikio makubwa yakipatikana yakiwemo kuimarika kwa majengo, huduma za elimu pamoja na miundombinu ya mawasiliano.
Ameahidi kuwa China itaendelea kushirikiana na Zanzibar na kutoa michango zaidi katika kusaidia uimarishaji wa uchumi wa Zanzibar.
Balozi Chen QiMan amemaliza muda wa utumishi hapa nchini, baada ya kuitumikia nafasi hiyo ya ubalozi mdogo kwa kipindi cha miaka miwili na nusu
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment