Monday, 26 August 2013

VITABU VITAKATIFU VISITUMIKE KUAPA


BAADHI ya wadau wanaoboresha Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wametaka Serikali itunge kitabu chake, ambacho viongozi wake watakitumia wakati wa kuapa katika utumishi wao badala ya kutumia vitabu vitakatifu kama Kurani ama Biblia.
Walidai hawaoni mantiki ya kutumia vitabu vya dini wakati utekelezaji wa majukumu yao hawafuati yale ya Mungu, ikiwemo kushindwa kuzuia ufisadi na wizi unaofanywa na viongozi hao.
Hayo waliyasema mwishoni mwa wiki wakati wakichangia Rasimu ya Katiba katika mkutano wa wananchi wa Jimbo la Mlalo mkoani Tanga, ulioandaliwa na Muungano wa Asasi za Kiraia Wilaya ya Lushoto (LUSCO) kwa ufadhili wa Shirika la The Foundation for Civil Society la jijini Dar es Salaam na kufanyika Kituo cha Walimu Mlalo (TRC).
"Serikali itafute kitabu chake kwa ajili ya viongozi wake kuapa, lakini wasitumie Biblia au Kuran kwani hawatekelezi mambo yaliyopo kwenye vitabu hivyo. Kama wangekuwa wanatekeleza yale yaliyoagizwa kwenye vitabu hivyo tungewakubali, mfano wezi wametakiwa kukatwa mikono na wazinifu kupigwa mawe hadi kufa.
"Lakini viongozi hao wanatakiwa kuwa na maadili na kulinda mali ya umma, lakini maagizo hayo ya Mungu hawayafuati kwanini washike Biblia au Kurani watakapokuwa na kitabu chao tutataka yale wanayoyatamka basi wayatekeleze kweli, sio kama wanavyofanya sasa kwenye vitabu vya dini," alisema Hazali Hazali (78), mkazi wa kijiji cha Mlalo.
Source:majira

No comments:

Post a Comment