Showing posts with label KATIBA. Show all posts
Showing posts with label KATIBA. Show all posts

Saturday, 21 September 2013

MAELFU YA WANANCHI WAJITOKEZA KATIKA MKUTANO WA CHADEMA,NCCR, CUF HUKO JANGWANI JIJINI DAR.


     Maelfu  wakazi wa jiji la Dar es salaam  wengi wao wakiwa ni  wafuasi wa vyama vya Chadema ,Cuf na NCCR Mageuzi  wemefurika katika  viwanja vya jangwani kuwasilikza  viongozi wakuu wa vyama hivyo ambapo kwa pamoja viongozi hao  wanapinga  hatua  ya serikali  kuingiza baadhi ya vipengele  katika mswada wa  sheria  ya marekebisho  ya  sheria  ya mabadiliko ya katiba .

Viongozi  hao  wanadai  kuwa  vipengele hivyo vitapelekea kupatikana kwa katiba  ya upande mmoja  na kuongeza kuwa kama mswada huo hautafanyiwa marekebisho, basi  wao  hawatashiriki katika bunge la katiba.
  
Katika viwanja hivyo  ulinzi uliimarishwa kutoka katika vikundi mbalimbali  vinavyomilikiwa na vyama hivyo  huku shamra shamra za huko na kule zikiwa hazikosekani ili mradi kunogesha mkutano.
 

Mwenyekiti wa taifa wa Chadema  na ambaye  ni kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni Mh Freeman Mbowe amewataka watanzania kuacha uoga na wasimame imara kudai katiba bora.
 

Naye mwenyekiti wa Cuf Mh Profesa Ibrahim Lipumba  amesema Tanzani inahitaji katiba ambayo italinda na kusimamia rasilimali za taifa  kuweza kutimia kwa usawa na kuzingatia mahitaji ya watanzania wenyewe.
 
Kwa upande wake mwenyekiti wa NCCR Mageuzi  na mbuge wa kuteuliwa amesema hakuna haja ya kutumia  mabavu  na badala yake ameitaka serikali itumie busara zaidi ili kuweza kufikia  mwafaka wa jambo hili.

Wednesday, 18 September 2013

CHIKAWE:HAKUNA SHERIA INAYOMBANA KIKWETE ASISAINI MSWADA WA SHERIA,MAANDAMANO YA WAPINZANI HAYATASAIDIA KITU



Waziri wa Katiba na Sheria, Mathis Chikawe amesema Rais Jakaya Kikwete hana mpango wa kuongeza muda wa uongozi wake baada ya 2015 kama baadhi ya wanasiasa wanavyodai. 

Kadhalika, waziri huyo amesema hakuna sheria inayomlazimisha Rais kusaini muswada wa sheria yoyote inayopitishwa na Bunge na wala inayoweka muda maalumu wa kutekeleza wajibu huo.
 

Akizungumza na gazeti hili jana, Chikawe alisema kwa vyovyote vile Rais Kikwete hawezi kuongeza muda wa kuwapo kwake madarakani kwa kuwa anaheshimu Katiba ya nchi iliyomuweka madarakani.
 

Waziri huyo alitoa kauli hiyo baada ya kutakiwa na gazeti hili kuzungumzia madai ambayo yamekuwa yakirudiwa mara kwa mara na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba kwamba amenasa taarifa za siri za kuwapo kwa mipango ya kuongeza muda wa Serikali ya sasa kukaa madarakani.
 

“Ngoja nikwambie ndugu yangu, watu wanaongea tu, kwanza Rais mwenyewe hana mpango huo, anasema kazi aliyonayo ni ngumu na haoni sababu ya kuongeza muda,”alisema Chikawe na kuongeza:
 

“Mara zote ukizungumza naye anasema tuharakishe mchakato wa Katiba na ikibidi tuingie katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 kama Katiba yetu inavyosema kwa kuwa kazi aliyofanya inatosha kabisa.”
 

Mapema mwezi Mei mwaka huu, Profesa Lipumba alisema kutokana na wasiwasi kwamba mchakato wa Katiba Mpya hautakamilika 2014, hivyo Uchaguzi Mkuu hautaweza kufanyika.
 

Kuhusu hatima ya Uchaguzi Mkuu iwapo Katiba Mpya itaanzisha mfumo wa Serikali tatu, Chikawe alisema: “Wananchi wasiwe na wasiwasi ikifika wakati huo kila kitu tutajua, lazima tutakuwa na sheria ya mpito ambayo itaweka mambo sawa mpaka kutufikisha katika Uchaguzi Mkuu.”


Rais kusaini muswada

Chikawe pia alizungumzia hatima ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Mpya ambapo alisema hakuna sheria inayomlazimisha Rais kusaini miswada inayopitishwa na Bunge.

“Hakuna sheria inayomlazimisha Rais asaini wala kumpa muda wa kusaini, mwenyewe anatumia busara na hekima tu katika kusaini sheria,”alisisitiza Chikawe.
 

Kauli ya Chikawe imekuja siku chache baada ya wenyeviti wa vyama vya CUF, NCCR -Mageuzi na Chadema kutoa tamko la kumtaka Rais Kikwete asisaini muswada huo mpaka pale yatakapokuwapo maridhiano ya wadau muhimu kuhusu muswada huo. 

Alisema kwa kutokusaini muswada huo, kunaweza kukaleta tafsiri mbili; kwanza ni wale wanaoweza kutafsiri kuwa ni dharau kwa wabunge waliopitisha muswada huo, kwamba walichofanya si sahihi na hakina maana.


Hoja ya pili alisema kwa kutosaini pia kunaweza kuzidisha msukumo kwa wanachama wa chama chake, lakini pia kutoka kwa wananchi ambao wanasubiri kwa hamu utekelezaji wa sheria hiyo.
 
Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa 2013 ambao ulipitishwa na mkutano wa Bunge uliopita baada ya mvutano mkali, umeendelea nje ya Bunge, huku kukiwa na madai kwamba ulipitishwa ukiwa na marekebisho ambayo yalifanyika kinyume na maoni ya wadau.
 
Madai mengine ni kwamba wabunge wa CCM waliongeza baadhi ya mambo kupitia majedwali ya marekebisho, hivyo kutoa mwanya kwa Serikali inayoongozwa na chama hicho kupitia kwa Rais kuwa na mamlaka zaidi ya uteuzi wa wajumbe husika.
 
Septemba 6 mwaka huu, wabunge wa CCM walitumia wingi wao kupitisha muswada huo katika mkutano wa Bunge ambao ulisababisha tafrani kiasi cha Mbowe na Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi kutolewa nje ya Bunge kwa amri ya Naibu Spika, Job Ndugai.
 
Katika tafrani hiyo, baadhi ya wabunge wa upinzani walirushiana makonde na askari wa Bunge, huku wabunge wote wa upinzani, isipokuwa Mbunge wa Vunjo (TLP), Augustine Mrema, wakisusia vikao vya muswada huo.

-Mwananchi

Monday, 16 September 2013

WAPINZANI WAUNGANA NA KUKUBALIANA KUFANYA MIKUTANO NCHI NZIMA ILI KUPINGA MCHAKATO WA KATIBA

 
VYAMA vya upinzani nchini, vimeamua kuungana ili kunusuru mchakato wa Katiba mpya. Msimamo huo ulitolewa jana jijini Dar es Salaam, wakati wenyeviti wa vyama hivyo ngazi ya taifa, walipofanya mkutano na waandishi wa habari.

Vyama vilivyofikia uamuzi huo ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kilichowakilishwa na Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, Chama cha Wananchi (CUF), kilichowakilishwa na Profesa Ibrahim Lipumba na Chama cha NCCR- Mageuzi, kilichowakilishwa na James Mbatia.

Wakati wa mkutano na waandishi wa habari, aliyesoma tamko lao ni Profesa Lipumba, ambaye alisema ushirikiano wao umelenga kuhakikisha Katiba mpya inapatikana kwa maslahi ya Watanzania.

Alisema kwamba, ushirikiano huo umetokana na Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Mpya kupitishwa bungeni Septemba 6, mwaka huu, kwa nguvu na wabunge wa CCM.

Alisema kuwa, muswada huo ulipitishwa ukiwa na kasoro mbalimbali, zikiwamo za CCM kuingiza vipengele bila kufuata utaratibu kwa maslahi yao na pia wananchi wa Zanzibar hawakushirikishwa ipasavyo.

“Muswada uliopelekwa bungeni, uliongezwa vifungu vingi ambavyo havikuwamo katika rasimu iliyopelekwa katika Serikali ya Zanzibar, kitendo hicho kinadhihirisha udanganyifu katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa katika suala la Katiba ya nchi inayotokana na wananchi.

“Sasa, yaliyojiri bungeni kwa siku tatu kuanzia Septemba 4 hadi 6, mwaka huu na yale yanayoendelea kusemwa na Serikali pamoja na CCM, ni mkakati wa kupitisha Katiba ambayo haikutokana na wananchi. Kwa maana hiyo, wenye nia njema na nchi, waunge mkono tamko hili,” alisema Profesa Lipumba.

Kutokana na kutoridhishwa na mchakato huo, wanasiasa hao walimtahadharisha Rais Jakaya Kikwete, asisaini muswada huo kwa kuwa marekebisho yaliyofanyika na taratibu zilizotumika kuupitisha, zilikwenda kinyume cha majadiliano na vyama na wadau yaliyofanyika mwaka 2011 na 2012.

Pia walimtaka Rais Kikwete kuurejesha muswada huo bungeni, ili ukafanyiwe marekebisho yatakayojenga tabia ya kuaminiana ili kuleta muafaka wa kitaifa wa mchakato wa mabadiliko ya Katiba.

“Tunaanza kuunganisha umma ili kufanya uamuzi mzito wa kunusuru mchakato wa Katiba mpya, ambao unaendelea kutekwa na kuhodhiwa na CCM na tunafanya hivyo kwa kuwa madaraka na mamlaka yote yapo kwa wananchi ambao Serikali inawajibika kwao,” alisema Profesa Lipumba.

Ili kuonyesha kuwa wapinzani hao hawaridhishwi na mchakato wa Katiba mpya, alisema Septemba 21, mwaka huu, utafanyika mkutano wa hadhara wa pamoja eneo la Viwanja vya Jangwani, Dare es Salaam.

Alisema mkutano huo utakuwa ni hatua ya mwanzo ya ratiba za vyama hivyo kuzunguka nchi nzima kuelezea masuala mbalimbali yanayohusu mchakato wa Katiba mpya.

Akizungumza baada ya tamko hilo, Mbatia alisema kama Rais Kikwete ataridhia mchakato huo haramu, uamuzi wake utakuwa ndiyo chanzo cha machafuko nchini.

Alimtahadhirisha Rais Kikwete asiusaini muswada huo kwa sababu anaweza kuandika historia mbaya ya jambo alilolianzisha kwa nia nzuri.

“Mkono wa Rais Kikwete ambao utashikilia kalamu, ndio utakaokuwa na hatma ya taifa hili, anaweza kujenga historia mbaya ya jambo ambalo amelianzisha mwenyewe, ninamuomba aweke maslahi ya taifa mbele kuliko chama chake.

“Mkono wake ukithubutu kusaini muswada huo, ajue ndio mwanzo wa machafuko, tunajua wapo wanaosema anakiharibia chama chake, lakini ajue tunampa ushauri wa bure ili atambue hagombei tena, hivyo hakuna sababu ya kuogopa mtu.

“Tunataka Katiba ya miaka 50 hadi 100 na ifahamike kwamba, Watanzania hawajawahi kuandika Katiba yao, hatutaki CCM kuhodhi na kuifanya ni mali yao.

“Itakumbukwa kwamba, Muungano wa Tanzania na Zanzibar ni tendo la siasa la maridhiano, hivyo hivyo tendo la Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar kati ya CCM na CUF lilifanyika kisiasa na ni la maridhiano.

“Tunaomba CCM waweke itikadi zao pembeni na wote tuseme Tanzania kwanza, siasa baadaye, maslahi ya taifa kwanza, chama baadaye, kwa kauli hiyo, tutapata Katiba mpya.

“Sisi tunashukuru Tume ya Jaji Warioba, kwani imefanya kazi nzuri na kuchukua mawazo ya kila kundi na vyama, yakiwamo ya Serikali tatu, sasa bila vyama vya siasa kuyasimamia haitapatikana Katiba ya Watanzania,” alisema Mbatia.


Mbowe anena
Naye Mbowe alisema haoni sababu uchaguzi wa mwaka 2015, ufanyike chini ya Katiba ya zamani na kuongeza kwamba katiba mpya itapatikana kwa njia yoyote ile.

Mbowe, ambaye alitumia muda mrefu kuwaonya waandishi wa habari, alilifananisha taifa na puto lililojaa upepo ambalo alisema halitakiwi kutobolewa na Rais Kikwete.

Alisema upepo huo ukitobolewa utasababisha machafuko ndani ya nchi na kumtaka Rais Kikwete kutafakari kwa kina kwa kurudisha muswada huo bungeni ili ukajadiliwe upya.

“Chadema hatutaki katiba ya zamani itumike wakati wa uchaguzi wa mwaka 2015, tutaitafuta Katiba mpya kwa njia mbalimbali hadi ipatikane.

“Tunataka kusonga mbele sio kurudi nyuma, hatutapona kama Katiba mpya hii itapitishwa na chama kimoja, naomba tuungane ili kuwa na sauti moja,” alisema.

Aliwataka waandishi wa habari wawe makini katika suala hili, kwa kuwa wao ni wadau muhimu katika kupata Katiba mpya bora.

Pamoja na hayo, alimzungumzia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Steven Wassira, kwamba amelewa madaraka na kwamba ndiyo maana anatoa kauli za kejeli kwa wapinzani.

Kwa mujibu wa Mbowe, Ikulu siyo mali ya Rais wala wasaidizi wake, bali ni ya Watanzania wote.

Alisema kamwe hawatarajii kwenda Ikulu juu ya suala hilo, bali watakwenda kwa wananchi ambao ndio wenye nguvu na maamuzi ya taifa hili.